Reli ya Standard Gauge inatazamiwa kukabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mtandao wa barabara baada ya serikali kufufua mipango ya kujenga barabara ya mwendokasi, itakayoendana bega kwa bega na reli hiyo.

Makampuni matatu sasa yanashindana kupata zabuni ya kujenga Barabara Kuu ya Nairobi-Mombasa yenye urefu wa kilomita 473, ambayo itatoa usafiri usiokatizwa wa magari kati ya miji hiyo miwili.

Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (KeNHA) inasema kuwa Shirika la Miundombinu na Ustawishaji wa Nchi za Nje ya Korea (KIND) ndiyo kampuni ya hivi punde zaidi kueleza nia ya zabuni ya mabilioni baada ya kuwasilisha Pendekezo la Uwekezaji wa Kibinafsi (PIIP) kwa ajili ya maendeleo ya barabara kuu.

Kampuni hiyo itashindania zabuni hiyo na kampuni ya Kimarekani ya Bechtel Executive, ambayo pia inatazamia zabuni ya faida kubwa ya mabilioni ya shilingi lakini sasa iko katika ushirikiano wa pamoja na Kampuni ya Uwekezaji wa Mitaji ya Marekani ya Everstrong Capital.