NAIROBI, 16 Juni 2021 (PSCU)
Shirika la Mama wa Taifa Margaret Kenyatta la Beyond Zero limepokea ruzuku ya shilingi milioni 1.3 kutoka kwa serikali ya Slovak ili kuimarisha kampeni zake dhidi ya nasuri.
Ruzuku hiyo ya shilingi milioni 1.3, iliyokabidhiwa shirika la Beyond Zero kupitia shirika la msaada la Slovak Aid, ilitiwa saini na Balozi František Dlhopolček na Mshirikishi wa shirika la Beyond Zero Bi Angella Langat siku ya Jumatano kwenye ubalozi wa Slovak Jijini Nairobi.
Ruzuku hiyo ni sehemu ya usaidizi ambao serikali ya Slovak imeendelea kuipatia sekta ya afya hapa nchini.
Awali, serikali ya Slovak ilifadhili upasuaji wa watoto kumi waliokuwa na maradhi ya moyo kwenye shughuli iliyotekelezwa na madaktari wa taifa hilo kwa ushirikiano na wenzao katika hospitali ya Mater Jijini Nairobi mwezi wa Machi mwaka 2019 na kushuhudiwa na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta.
Hii ilifuatiwa na msaada uliokabidhiwa Ofisi ya Mama wa Taifa wa vifaa vya kukabiliana na Janga la Covid-19 wa thamani ya shilingi milioni 26 mwezi Julai mwaka jana ambao ulihusisha vifaa vya kupima, vifaa vya kujikinga, vifaa vya kusaidia kupumua, vyeuzi, mavazi na viatu.
Akizungumza katika sherehe hiyo fupi ya kutiwa saini, Balozi Dlhopolček alisema ofisi yake inanuia kushirikiana zaidi na shirika la Beyond Zero hususan kukabiliana na matatizo ya kina mama wanaougua kutokana na nasuri.
“Huu ndio mradi wa kwanza wa shirika la Beyond Zero ambao utafadhiliwa na shirika la msaada la Slovak Aid. Lakini nadhani huu ndio mwanzo kwa sababu katika sera yetu, Kenya ni miongoni mwa mataifa ambayo shirika hili la msaada limetoa kipaumbele.
“Tunatazamia kushirikiana zaidi na shirika la Beyond Zero kwa sababu tunatambua yale mnayoyafanya na tunamuona Mama wa Taifa kuwa muimarishaji wa ushirikiano wetu,” kasema Balozi Dlhopolček.
Alitoa mfano wa afya, kilimo na elimu kuwa baadhi ya Nyanja kuu ambazo taifa lake linaangazia hapa nchini.
Kwa upande wake Bi Langat, aliipongeza Slovakia kwa msaada huo wa kifedha kwa shirika la Beyond Zero huku akisema utasaidia sana kina mama wanaougua nasuri.
“Tutatenga fedha hizo kufanikisha mpango wa kupeleka mashinani huduma za afya katika eneo la kaskazini ambako kuna visa vingi vya ugonjwa huo kutokana na kiwango cha chini cha kufikia vituo vya afya na umaskini, ” kasema Bi Langat.
Hafla hiyo ya kutia saini ruzuku hiyo ilishuhudiwa na Naibu Balozi wa Slovakia Kamila Kukova na Msimamizi Mkuu wa Mawasiliano katika Ofisi ya Mama wa Taifa Bi Vivianne Ngugi.
-Tamati-
More Stories
Mwanahabari Mkongwe Leonard Mambo Mbotela Aapishwa
“Nimewasikia wakijaribu kusema wana idadi fulani, kwa hakika, kama huwezi hata kupata mgombea wa spika wa Seneti, una idadi gani?” Rais Ruto