Septemba 23, 2021 (PSCU) –Rais Uhuru Kenyatta amewasili katika Kambi ya Manda Bay ya Jeshi la Wanamaji nchini iliyoko katika Kaunti ya Lamu.
Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Ulinzi nchini ataongoza sherehe ya kukabidhi bendera za kutambulisha Kikosi cha kambi hiyo ya Jeshi la Wanamaji nchini katika Kaunti ya Lamu.
Hafla hiyo ya kihistoria itakipandisha hadhi kikosi hicho cha Manda Bay na kukipa uhuru wa kujisimamia kama kituo maalaum cha kijeshi chenye uwezo wa kushughulikia maslahi ya kitaifa, kanda na ya kimatifa.
Vile vile, Rais atazindua hospitali itakayoshughulikia maafisa wa kijeshi ambao huenda wakajeruhiwa wakati wa oparesheni za kiusalama.
Hospitali hiyo pia itawahudumia maafisa wengine wa usalama nchini ambao watakakuwa wakihudumu katika eneo la Kaskazini mwa Pwani ya Kenya hadi katika mpaka wa Kenya na Somalia.
Hospitali hiyo yenye vitanda 14 itatoa huduma za dharura kwa majeruhi kabla ya kuwapa rufaa ili kupata matibabu maalum zaidi kwingineko iwapo kutatokea dharura ya kufanya hivyo.
Rais anaandamana na Waziri wa Ulinzi Balozi Dkt Monica Juma, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi nchini Jemedari Robert Kibochi na makamanda wa vikosi mbali mbali vya kijeshi nchini na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini.
More Stories
LAMU HADI NAIROBI
JUMBA LA KUMBUKUMBU CHINI YA MAJI
DAR ES SALAAM.